USHIRIKIANO KATI YA VYUO VYA TVET TANZANIA NA CHINA WAENDELEA KUIMARIKA
Tanzania na China zimeendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET), ikiwa ni sehemu ya juhudi za pamoja za kukuza ujuzi, maarifa na ubunifu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa pande zote mbili.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Fredrick Salukele, wakati akifungua semina ya kubadilishana uzoefu na ujuzi kati ya vyuo vya TVET kutoka Tanzania na China, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Adolf Mkenda. Semina hiyo imefanyika tarehe 11 Julai 2025 katika Ofisi za NACTVET, Kanda ya Mashariki, Dar es Salaam.
Dkt. Salukele alisema kuwa ushirikiano huu ni sehemu ya dira ya pamoja ya kujenga bara la Afrika kupitia elimu yenye msingi wa ujuzi. Alisisitiza kuwa semina hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya dhati ya pande zote mbili katika kukuza ushirikiano endelevu kwenye elimu ya ufundi.
Akizungumzia mafanikio ya ushirikiano huu, Dkt. Salukele alibainisha kuwa semina ya nne iliyofanyika mwaka 2024 iliwezesha Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) na Chuo cha Ufundi Arusha (ATC) kusaini mikataba ya ushirikiano na vyuo 10 kutoka China. Aidha, wafanyakazi 12 wa Baraza la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) walipata fursa ya kutembelea China kwa ajili ya kujifunza mifumo bora ya uendeshaji wa elimu ya TVET.
Kwa upande wake, China imeahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa kina zaidi katika maeneo muhimu kama vile:
- Kubadilishana wataalamu;
- Kuandaa mitaala ya pamoja;
- Kuandika na kuchapisha vitabu vya kujifunzia na kufundishia;
- Kuanzisha programu za mafunzo zinazoendana na viwango vya kimataifa na mahitaji ya soko la ajira.
Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la NACTVET, Bi. Bernadetta Ndunguru, alieleza kuwa Baraza litaendelea kuhakikisha kuwa elimu ya TVET inayotolewa nchini Tanzania inazingatia viwango vya ubora na inajibu ipasavyo mahitaji ya soko la ajira kitaifa na kimataifa.
Ujumbe kutoka China ulioongozwa na Prof. Yu Xiaoqi, Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Elimu kutoka Mkoa wa Sichuan, ulieleza kuwa China itaendelea kushirikiana na Tanzania, hususan katika kuimarisha elimu ya TVET. Aidha, alieleza kuwa hatua za awali zimeanza kuchukuliwa kuleta programu za teknolojia ya kisasa kama vile Akili Bandia (AI) ili kuboresha zaidi utoaji wa elimu ya ujuzi nchini.
Semina hiyo ambayo ni ya tano kufanyika nchini Tanzania, imewaleta pamoja wataalamu kutoka vyuo mbalimbali vya TVET kutoka Tanzania na China kwa ajili ya kubadilishana uzoefu wa kitaaluma, kujadili changamoto, mafanikio, na fursa mpya za kuimarisha elimu ya ufundi.Ushirikiano huu unaendelea kuwa mfano bora wa namna elimu ya ufundi inaweza kuwa daraja la maendeleo kati ya mataifa, huku ikiwajengea vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika soko la ajira la kitaifa na kimataifa.
MAGEUZI KATIKA ELIMU YA UFUNDI NA MAFUNZO YA UFUNDI STADI
Kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023), Serikali ya Tanzania imeweka msukumo mkubwa katika kuhakikisha elimu ya TVET inapata hadhi inayostahili na kuwa miongoni mwa njia kuu za kukuza ajira na ujuzi kwa vijana na taifa.
Sera hii mpya inatambua kuwa elimu ujuzi ni nguzo muhimu ya maendeleo ya viwanda, biashara, kilimo na huduma mbalimbali. Kwa msingi huo, Serikali imewekeza zaidi katika miundombinu ya vyuo vya TVET, kuongeza walimu na wakufunzi wenye sifa, na kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi, kama China, katika kubadilishana teknolojia, maarifa na mbinu za kufundishia.