NACTVET YAKUTANA NA KAMATI YA UDAHILI WA PAMOJA KOZI ZA AFYA NA SAYANSI SHIRIKISHI
Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limekutana na wadau wake wakiwemo; mjumbe kutoka ofisi ya Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Bi. Asnath Mpelo, mabaraza ya kitaaluma, Wakuu wa Taasisi/Vyuo vya Afya na Sayansi Shirikishi, leo tarehe 24 Julai, 2025 katika mkutano wa saba wa Kamati ya Udahili wa Pamoja kwa kozi za Afya na sayansi shirikishi jijini Dodoma.
Mkutano huo ni sehemu ya kutathmini mwenendo mzima wa zoezi la udahili wa pamoja (CAS) awamu ya kwanza, ambapo wajumbe pia wamejadili mafanikio na changamoto zilizojitokeza ili kubaini na kupendekeza maeneo yanayohitaji maboresho katika madirisha yatakayoendelea.
Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Lingwanda amefungua rasmi mkutano huo wa saba na kupongeza wajumbe wa Kamati ya Udahili wa Pamoja (CAS) na Menejimenti ya NACTVET kwa ushirikishwaji katika udahili unaoendelea kwa lengo la kuendelea kuboresha viwango na ujuzi kwa mhitimu.
Dkt.Lingwanda amewarai wadau kusimamia miongozo ya Baraza na kuhakikisha wanazingatia viwango vya ubora katika maeneo yote ya utoaji wa mafunzo na kutumia kikamilifu mifumo rasmi ya udahili iliyoidhinishwa.
Aidha, Dkt. Lingwanda amesisitiza umuhimu wa vyuo kuwasilisha taarifa sahihi za udahili wa wanafunzi kwa wakati sambamba na mwenendo wa maendeleo ya wanafunzi na idadi yao, ili kuhakikisha kunakuwepo uwazi na usimamizi bora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini.
Mkutano huo wa siku moja wa Kamati ya Udahili wa Pamoja ni sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa dirisha la udahili wa wanafunzi wa Astashahada na Stashahada kwa mwaka wa masomo 2025/2026, na hufanyika kila mwaka kwa mujibu wa kalenda ya Baraza. Lengo kuu la Kamati ya Pamoja ni kuhakikisha shughuli za udahili zinaendeshwa kwa ufanisi na uwazi na kwa kufuata taratibu na miongozo ya Baraza.