Tarehe 27 Aprili, 2026, Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Dkt. Mwajuma Ibrahim Lingwanda, amefungua mafunzo kwa walimu 131 wa masomo ya amali katika shule za sekondari.
Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea walimu hao uwezo wa mbinu shirikishi za ufundishaji unaozingatia umahiri, kutafsiri mitaala na upimaji na yanatolewa katika Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro (MVTTC) kuanzia tarehe 27 hadi 29 Aprili, 2026.
Dkt. Lingwanda amesema, Baraza linatambua walimu kama mhimili muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023, hivyo ni muhimu kuendelea kuwajengea uwezo ili kuboresha ufundishaji unaozingatia umahiri.
Akitoa salamu kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Morogoro, Afisa Taaluma Bw. Tullo Fundi, aliwashauri walimu kutumia fursa hiyo ya mafunzo kuongeza uwezo wa kujifunza na kuchangamkia fursa mbalimbali za kujiendeleza ikiwemo zinazopatikana kwa njia ya masafa.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha MVTTC, Bw. Samwel Kaali, amesema kuwa chuo hicho kimejipanga vyema kuhakikisha walimu wanapata mafunzo bora yatakayowawezesha kuboresha ufundishaji wa mafunzo ya amali.

