Wadau wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (TVET) kwa programu za Afya na Sayansi Shirikishi wamekutana kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Mwongozo wa Usimamizi, Tathmini na Mitihani kwa programu za Afya na Sayansi Shirikishi katika vyuo vya TVET nchini.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Dkt. Mwajuma Lingwanda, amefungua warsha hiyo leo tarehe 23 Februari,2026 jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Dkt. Lingwanda amesema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa zoezi la ugatuzi wa usimamizi na uendeshaji wa mitihani ya Kada ya Afya katika ngazi ya Astashahada na Stashahada kwenda kwenye Kanda za Uratibu wa Mitihani ikiwa ni hatua mojawapo ya kuvijengea vyuo uwezo wa kuendesha mitihani yake vyenyewe.
Amesema mwongozo huo unalenga kuweka mfumo thabiti wa upangaji, usimamizi na uthibiti wa tathmini na mitihani katika vyuo vya Afya na Sayansi shirikishi, pamoja na kuhakikisha uwazi na uwajibikaj katika mchakato mzima wa uendeshaji mitihani.
“Ni muhimu kwa washiriki kutumia fursa hii kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha mwongozo huu, ambao utafafanua majukumu ya kila mmoja na kuleta ufanisi katika zoezi la tathmini na mitihani ili hatimaye kuongeza umahiri wa wahitimu pamoja na kuboresha ubora wa mafunzo yanayotolewa,” amesema.
Sheria ya Baraza, Sura ya 129, Kifungu cha 9(d), kinaipa Baraza jukumu la kuweka utaratibu wa kusimamia na kuendesha mitihani katika vyuo vya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi nchini.

