Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Idara ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, imekutana na Menejimenti ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kujadili na kuweka mikakati ya kuimarisha uratibu wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VET) nchini.
Kikao hicho kimeongozwa na Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Fredrick Salukele, tarehe 11 Mei, 2026 katika ofisi za NACTVET Makao Makuu jijini Dodoma.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Salukele amesema, Wizara imeona umuhimu wa kukutana na taasisi hizo mbili ili kujadili kwa kina masuala yahusuyo majukumu ya kila taasisi kisheria, changamoto za kiutekelezaji na namna ya kushirikiana katika uratibu na utekelezaji wa majukumu kwa kuzingatia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 Toleo la 2023.
Masuala yaliyojadiliwa ni pamoja na usajili wa vyuo vya VET, uandaaji wa mitaala inayoendana na mahitaji ya soko la ajira, udahili, tathmini na utunuku, uandaaji wa miongozo mbalimbali ya utoaji wa mafunzo pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za mafunzo na viwanda.
Aidha, kikao hicho kimefikia makubaliano mbalimbali yenye lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi, uratibu na utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi nchini ili kuzalisha wahitimu wenye ujuzi na umahiri wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira kimataifa na kuchangia katika maendeleo ya taifa.

