Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limevitaka vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini kuzingatia kikamilifu taratibuza udahili na mitihani ili kuepusha athari kwa wanafunzi na Taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo Februari 4, 2026, na Dkt. Obeid Mahenya, Meneja wa Utahini na Utunuku wa NACTVET kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa NACTVET wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa Maafisa Udahili na Mitihani kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar katika Ukumbi wa NSSF, mkoani Shinyanga.
Dkt. Mahenya amesema elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ni nguzo muhimu katika kukuza rasilimali watu wenye ujuzi, kuchochea ajira na kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2025–2050 na hivyo ni muhimu kuzingatia taratibu na miongozo iliyowekwa.
Alibainisha kuwa NACTVET imebaini changamoto za udahili hafifu katika kanzidata yaBaraza pamoja na ucheleweshaji wa upakiaji wa matokeo ya mitihani, haliinayosababisha changamoto mbalimbali kwa wanafunzi ikiwemo kuchelewa kuendelea na ngazi mbalimbali za masomo na kupata vyeti kwa wakati.
Dr. Mahenya amesema kikao kazi hiki kinalenga kuwajengea uwezo Maafisa Udahili na Mitihani, kubadilishana uzoefu, kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki, na kuboresha ufanisi katika usimamizi wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi.

