Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) limetoa semina elekezi kwa wajumbe wapya wa Bodi za Masomo (Subject Boards) kwa lengo la kuwajengea uelewa kuhusu kazi za Baraza na wajibu wao, ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Akizungumza wakati wa semina hiyo iliyofanyika jijini Dodoma leo tarehe 20 Aprili, 2026, Katibu Mtendaji wa NACTVET, Dkt. Mwajuma Ibrahim Lingwanda, amesema Bodi hizo zina jukumu kubwa la kuhakikisha mafunzo yanayotolewa yanakidhi mahitaji ya soko la ajira. Amesisitiza kuwa Bodi hizo zinapaswa kuhakikisha kuwa uandaaji wa mitaala unashirikisha waajiri na wadau wengine ili kubaini mahitaji halisi ya soko la ajira.
“Bodi hizi ni msingi wa utekelezaji wa majukumu yetu, na ufanisi wake utachangia kwa kiasi kikubwa ubora wa wahitimu wanaozalishwa katika mfumo wa TVET,” amesema.
Ameeleza kuwa Sheria ya NACTVET inaipa Baraza mamlaka ya kuanzisha Bodi hizo za Masomo na kuzipatia majukumu mahsusi. Aidha, alizitaja Bodi zilizopo kwa sasa kuwa ni Bodi ya Afya na Sayansi Shirikishi (HAS), Bodi ya Sayansi na Teknolojia Shirikishi (SAT) na Bodi ya Biashara, Utalii na Mipango (BTP,) ambazo kila moja inaundwa na wajumbe saba kutoka katika taasisi za TVET, vyuo vikuu na waajiri.
Dkt. Lingwanda amewasihi wajumbe hao kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uadilifu, huku wakitoa michango yao ya kitaalamu kwa kuzingatia umuhimu wa TVET kama nguzo ya maendeleo ya ujuzi nchini, katika kukuza viwanda, kuongeza ajira na kuendeleza ubunifu kulingana na mahitaji ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Huduma za Vyuo, Dkt Magreth Shawa, alisema miongoni mwa majukumu ya msingi ya Bodi hizo ni kupitia masuala muhimu ya kitaalamu na kuwasilisha mapendekezo kwa Baraza la Uongozi kwa ajili ya idhini. Aliongeza kuwa wajumbe wa Bodi hizo wanatarajiwa kuhudumu katika nafasi zao kwa miaka mitatu.

