Mashindano ya Ujuzi Kitaifa 2026 yameanza rasmi kwa hatua ya mchujo ngazi ya Kanda, yakiwakutanisha wanafunzi wa vyuo vya elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kutoka maeneo mbalimbali nchini kuchuana katika fani mbalimbali za ujuzi. Mashindano hayo yalifanyika kuanzia tarehe 8 hadi 17 Juni, 2026 katika vituo vitatu vya mashindano vilivyopo Dar es Salaam, Dodoma na Arusha.
Mashindano hayo yalianza tarehe 8 Juni, 2026, kwa fani ya Upishi, ambapo wanafunzi walishiriki mchujo wa ngazi ya kanda uliofanyika katika Chuo cha VETA cha Hoteli na Utalii mkoani Arusha. Tarehe 9 Juni, 2026, wanafunzi wa fani za Uhandisi wa Mitambo na Uwekaji wa Vigae Ukutani na Sakafuni walishiriki mashindano hayo yaliyofanyika katika Chuo cha Ufundi Arusha na Chuo cha Ufundi Don Bosco, Dodoma.
Tarehe 10 Juni, 2026, mashindano yaliendelea kwa fani za Uchomeleaji na Uungaji Vyuma pamoja na Ushonaji, Ubunifu na Teknolojia ya Nguo, ambapo mchujo ulifanyika katika Chuo cha VETA Dodoma na Anna Fashion Academy, Dar es Salaam. Aidha, tarehe 11 Juni, 2026, wanafunzi wa fani ya Mtandao wa Vitu (IoT) walishiriki mashindano katika Chuo cha Ufundi Arusha, huku washiriki wa fani ya Ufundi Umeme wakichuana tarehe 13 Juni, 2026 katika Chuo cha VETA Dodoma.
Mashindano hayo yaliendelea tarehe 15 Juni, 2026 kwa fani ya Urembo Tiba katika Manjano Beauty Academy, Dar es Salaam, na kuhitimishwa tarehe 16 Juni, 2026 kwa fani ya Mekatroniki katika Chuo cha VETA Kipawa, Dar es Salaam.
Mashindano haya yanaratibiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Mashindano ya ngazi ya Kanda yanatumika kama hatua ya mchujo kwa ajili ya kupata washiriki watakaoshiriki Mashindano ya Ujuzi Kitaifa yatakayofanyika jijini Tanga kuanzia tarehe 15 hadi 24 Agosti, 2026.
Kila fani ilitoa washindi watano bora waliofanikiwa kufuzu kushiriki Mashindano ya Ujuzi Kitaifa 2026. Washindi hao watashindana katika ngazi ya taifa kuwania nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya ujuzi ngazi ya Afrika na baadaye katika mashindano ya kimataifa. Haya ni mashindano ya kwanza kufanyika nchini tangu Tanzania ipate uanachama wa WorldSkills Africa, hatua inayofungua fursa kwa vijana wa Kitanzania kushiriki, kuonesha uwezo wao na kujipima katika viwango vya kimataifa vya ujuzi.
Mkurugenzi wa Uthibiti Ubora wa NACTVET, Dkt. Jofrey Oleke, alisema kuwa mashindano hayo yanalenga kuhamasisha maendeleo ya ujuzi miongoni mwa vijana kupitia elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira. Dkt. Oleke aliongeza kuwa mashindano hayo pia yanatoa fursa kwa washiriki kujipima uwezo wao, kujifunza kutoka kwa wenzao na kujiandaa kwa ushindani katika ngazi za juu zaidi.
Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa mashindano hayo, Prudence Musoni, alisema kuwa ushiriki wake umemwezesha kujifunza mbinu mpya za upishi, kuongeza uzoefu wa vitendo na kuimarisha uwezo wake kitaaluma.
Mashindano ya Ujuzi Kitaifa yanatarajiwa kuwa chachu ya kuibua vipaji, kuhamasisha ubunifu na kuimarisha ubora wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi nchini, huku yakitoa jukwaa kwa vijana wenye ujuzi kuonesha uwezo wao na kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya ujuzi ngazi ya Afrika na kimataifa.

